9 Februari 2022 - 10:37
Indhari kuhusu aina mpya ya Virusi vya Ukimwi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kupambana na UKIMWI, UNAIDS limesema utafiti upya uliochapishwa kutoka nchini Uholanzi umeonesha kuwepo kwa spishi mpya ya kirusi cha UKWIMI ambacho licha ya kusambaa kwa kasi pia kina madhara zaidi.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Taarifa ya UNAIDS kutoka Geneva, Uswisi imeeleza kuwa watu wanaoishi na aina mpya ya Virusi Vya UKIMWI - VVU hali zao za mwili hudhoofika mara mbili ya kiwango cha kupungua kwa kinga mwili ( CD4), pia wana viwango vya juu vya virusi vya UKIMWI  (kiasi cha virusi kwenye damu) na wanakuwa hatarini kusambaza haraka VVU mara mbili hadi tatu baada ya kugundulika ikilinganishwa na kirusi cha zamani cha UKIMWI.

Utafiti huo, ulioongozwa na Chuo Kikuu cha Oxfords katika Taasisi yake ya  Takwimu, ulikuwa wa kwanza kugundua spishi ndogo ya B ya virusi. Utafiti huo pia umebaini kuwa aina hiyo imekuwa ikisambazwa nchini Uholanzi kwa miaka mingi na imekuwa ikipokea matibabu ya VVU.

Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS Eamonn Murphy amesema watu milioni kumi wanaishi na VVU duniani kote lakini bado hawapati matibabu, na hivyo kuchochea kuenea kwa virusi hivyo na uwezekano wa kuwepo kwa aina nyingine.

Murphy anasema kuna udharura wa kupeleka ubunifu wa hali ya juu wa matibabu kwa njia zinazofikia jamii zenye uhitaji zaidi iwe ni matibabu ya VVU au chanjo ya COVID-19. Virusi vya UKIMWI au VVU ndio janga kuu zaidi la wakati huu, inakadiriwa kuwa watu milioni 79 wameambukizwa virusi hivyo, ambavyo bado hakuna chanjo na hakuna tiba.

Takriban watu milioni 36 wamekufa kutokana na magonjwa yanayohusiana na UKIMWI tangu kuanza kwa janga hilo na watu wapya milioni 1.5 waliambukizwa VVU mwaka 2020.

342/